AJIBU kutinga rasmi YANGA leo
KOCHA GEORGE LWANDAMINA.
BAADA ya kukamilisha usajili wake wa kujiunga na klabu ya Yanga, mshambuliaji Ibrahim Ajibu, pamoja na wachezaji wengine wapya wa timu hiyo, leo wanaanza rasmi kazi ndani ya kikosi cha kocha George Lwandamina.
Akizungumza na Nipashe jana, Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema mazoezi hayo yatakuwa chini ya Lwandamina na wanategemea kuwa na nyota wao wote isipokuwa wale waliopo kwenye kikosi cha timu ya Taifa 'Taifa Stars'.
"Mazoezi yatafanyika Shule ya Sekondari ya Loyola, wachezaji wote waliosajiliwa wataungana na wenzao kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu," alisema Hafidh.
Nipashe inafahamu mashabiki wengi wa klabu hiyo watataka kumuona kwa mara ya kwanza nyota wao mpya, Ajibu aliyesajiliwa na timu hiyo akitokea Simba.
Akizungumza na Nipashe jana, Ajibu alisema anafurahi kuona kesho anaanza rasmi kuitumikia timu yake mpya na anategemea kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wachezaji wenzake.
"Nataka akili yangu kuielekeza kwenye timu yangu mpya, nipo tayari kuanza kuitumikia na naamini mambo yataenda sawa," alisea Ajibu.
Yanga inaanza mazoezi kwenye uwanja wa huo wa Loyola huku benchi la ufundi likiwa limepeleka mapendekezo ya kuweka kambi nje ya Dar es Salaam ili kupata utulivu katika maandalizi yao

Comments
Post a Comment