HAYA NDIYO MANENO YA KOCHA TAIFA STARS

KOCHA SALUM MAYANGA

TIMU ya soka ya Taifa (Taifa Stars) inavaana na Rwanda (Amavubi) katika mchezo wa marudiano kuwania nafasi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) huku kocha Salum Mayanga akisema timu hiyo ina nafasi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo. 

Akizungumza na gazeti hili kutoka Rwanda, Mayanga, alisema kuwa pamoja na matokeo ya sare ya bao 1-1 waliyoyapata kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa jijini Mwanza, Taifa Stars bado ina uwezo wa kufanya vizuri katika mchezo wa leo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Nyamirambo. 

“Matokeo ya Mwanza hayajatukatisha tamaa, tumejiandaa kwa mchezo wa leo na niseme tu kuwa tunayo nafasi ya kusonge mbele kama wachezaji watapambana na kufuata maelekezo yote,” alisema Mayanga. 

Kocha huyo alisema pia hatarajii kufanya mabadiliko katika kikosi kilichocheza wiki iliyopita na wamepanga kuanza kwa kasi baada ya sasa kuwafahamu vyema wapinzani wao. 

“Tunataka kumaliza kazi ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, tutacheza mchezo wa kasi kwa kuwa tunajua na wao (Rwanda) wataingia kwa kasi ili kutupa presha na sisi tutakuwa makini pia kwenye safu yetu ya ulinzi,” aliongeza kusema Mayanga. 

Katika mchezo wa leo, Taifa Stars inahitaji ushindi wa aina yoyote au matokeo ya sare ya kuanzia mabao 2-2 ili kuweza kuwatupa nje Rwanda na kusonga mbele. 

Mshindi katika mechi hiyo itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Rwanda atakutana na mshindi wa mchezo kati ya Uganda dhidi ya Sudan Kusini. 

Mara ya mwisho Taifa Stars kushiriki kwenye fainali za CHAN ilikuwa ni mwaka 2008 katika michuano ya kwanza iliyofanyika Ivory Coast wakati huo Taifa Stars ikiwa chini ya Kocha Mbrazil Marcio Maximo.

Comments

Popular posts from this blog

Kubemenda Mtoto

Siwezi pitisha siku bila kutembea na malaya

HAYA NDIO MADHARA YA KUFANYA MAPENZI KWA NJIA YA MDOMO. (Oral sex).