Hatimaye yanga wafuata uchawi wa simba


BAADA ya kufanya mazoezi ya wiki moja jijini Dar es Salaam, kikosi cha timu ya Yanga kinaondoka leo kuelekea Morogoro, sehemu ambako Simba ilipatia makali yake ya kuongoza Ligi Kuu kwa muda mrefu kabla ya Wanajangwani hao kuwapiku na kutwaa ubingwa. 

Kambi hiyo ya Yanga ni kwa ajili ya kujiwinda na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba itakayochezwa Agosti 23, mwaka huu pamoja na Ligi Kuu Bara itakayoanza siku tatu baada ya mchezo huo. 

Yanga jana ilifanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam yaliyoanza saa 8:30 mchana. 

Afisa habari wa klabu hiyo, Dismas Ten, alisema kuwa timu hiyo itakaa Morogoro mpaka Agosti 5 na kisha kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Singida United na kuendelea kufanya mazoezi mpaka Agosti 11 ambapo siku inayofuata itacheza mchezo mwingine wa kirafiki kabla ya kuondoka Agosti 13 kwenda kuendelea na kambi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba. 

Kambi hiyo ni mapendekezo ya kocha George Lwandamina ambaye anaendelea kuwanoa wachezaji wake. 

Zulu kutemwa Kiungo Papy Tshishimbi tayari ana uhakika wa kupewa mkataba wa miaka miwili kuichezea timu hiyo, hali hiyo inaifanya Yanga kutokuwa na nafasi nyingine kwa ajili ya mchezaji wa kimataifa. 

Tshishimbi amechukua nafasi ya kiungo Haruna Niyonzima aliyetimkia Simba wakati kipa Youthe Rostand amefanya kutokuwapo na nafasi nyingine kwa mchezaji wa kigeni. 

Hata hivyo, Yanga inawafanyia majaribio mabeki Henry Okoh kutoka Nigeria pamoja na Mghana Fernando Bongyang kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Vincent Bossou aliyeachana na timu hiyo. 

Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo aliliambia Nipashe kuwa mchezaji mmoja kati ya wawili hao atakayemridhisha Kocha Lwandamina anaweza akasajiliwa baada ya Yanga kuvunja mkataba wa Justine Zulu. 

"Mkataba wa Zulu na Yanga unamalizika Novemba mwaka huu, hapa kuna mawili tunafikiria, moja kuvunja mkataba na Zulu ili mchezaji mmoja kati ya Okoh na Bongyang asajiliwe, au tusubiri mpaka dirisha dogo la usajili ambapo mkataba wake utakuwa umeisha ndipo tusajili mchezaji mmoja kati ya hawa wanaofanya majaribio," alisema kiongozi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini. 

Alisema kiungo mkongomani kutoka klabu ya Mbabane Swallows, Tshishimbi yeye atasajiliwa moja kwa moja na anategemewa kusaini mkataba muda wowote.

Comments

Popular posts from this blog

Kubemenda Mtoto

Siwezi pitisha siku bila kutembea na malaya