OKWI AIFUATA SIMBA SOUTH


MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Simba kutoka Uganda, Emmanuel Okwi, ametua kambini Afrika Kusini jana na kuwaambia mashabiki wa timu hiyo wajiandae kuona "vitu vyake" katika mechi ya kirafiki dhidi ya Rayon FC itakayofanyika Agosti 8 mwaka huu (Simba Day) kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Saalam. 

 Okwi, alisema kuwa mbali na kuchelewa kujiunga na kambi ya timu hiyo, yuko katika kiwango kizuri na benchi la ufundi halitakuwa na kazi kubwa kuinua kiwango chake. 

Okwi amewaambia mashabiki na wanachama wa Simba wawe watulivu, amejiandaa kuwapa kile wanachokitarajia kutoka kwake na anafahamu vizuri ndoto za klabu hiyo yenye makao makuu yake Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini. 

"Ninaenda Sauzi leo (jana), nitakuwa Dar es Salaam siku ya Simba Day, najua watu wanahamu ya kuniona, mashabiki wawe watulivu," alisema kwa kifupi mshambuliaji huyo kutoka SC Villa ambaye anawania kiatu cha dhahabu katika Ligi Kuu ya Uganda. 

Nyota wengine wapya ambao wanadaiwa kusajiliwa na Simba na bado hawajaripoti kwenye kambi hiyo ni kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima ambaye anashiriki kozi ya ukocha ngazi ya leseni C inayotambulika na Shirikisho la Soka Tanzania (CAF) huku kipa Aishi Manula naye akisubiri muda mwafaka wa kuanza maisha mapya Msimbazi. 

Pia mshambuliaji bora wa Ligi Kuu Ghana, Nicolas Gyan ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili katika klabu hiyo pia bado hajajiunga kwenye kambi ya timu hiyo huku ikielezwa kuwa anakamilisha baadhi ya majukumu na klabu yake ya Dwafts ya nchini humo. 

Wakati huo huo meneja wa timu hiyo, Abbas Ally, amesema kuwa wachezaji wa timu hiyo wanaendelea vizuri na mazoezi ambayo yanafanyika kwa awamu mbili kila siku. 

"Kila kitu kiko sawa mpaka leo, programu za mwalimu zinakwenda vyema na wachezaji wanaonyesha ushindani kila kukicha, ni ishara ya kuanza kusaka namba kwenye kikosi cha kwanza," alisema meneja huyo. 

Simba inatarajia kucheza mechi mbili za kirafiki na klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini ambazo ni Orlando Pirates na Bidvest Wits huku ikitarajia kurejea nyumbani Agosti 5 mwaka huu.

Comments

Popular posts from this blog

Kubemenda Mtoto

Siwezi pitisha siku bila kutembea na malaya

HAYA NDIO MADHARA YA KUFANYA MAPENZI KWA NJIA YA MDOMO. (Oral sex).