KIMYA KIMYA:Mkameruni anaesubiria ripoti ya LWANDAMILA kukamilisha usajili YANGA.

ZAINAB IDDY NA SALMA MPELI

WAKATI Simba wakikwea pipa alfajiri ya leo kwenda Afrika Kusini kuweka kambi ya wiki mbili, watani zao wa jadi Yanga wanamalizana na kiungo mkabaji Fernando Bongnyang na kuendelea na mazoezi yao jijini Dar es Salaam.

Simba na Yanga zinataraji kukutana Agosti 23 mwaka huu katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2017/18.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika ambaye amereja nchini jana akitokea Rwanda na Uganda, amesema wanasubiri ripoti ya kocha George Lwandamina ili kukamilisha usajili wa kiungo huyo raia wa Cameroon.

Bongnyang anayetokea katika klabu ya Cotton Sports ya nchini humo, alitua nchini wiki iliyopita na inaelezwa tayari ameshamvutia Lwandamina kuchukua nafasi ya Justine Zulu ambaye huenda akaondoka kikosini.

Katika kuhakikisha wanatimiza azma yao kuifunga Simba, Lwandamina ameamua kuongeza dozi katika kikosi chake kwa kufanya mazoezi ya gym pamoja na uwanjani kwa siku moja.

Awali, Lwandamina alianza mazoezi ya uwanjani Jumanne iliyopita kabla ya kuhamia gym timu ilipofanya kwa siku nne, huku jana Jumapili wakifanyiwa vipimo vya misuli ili kuona iwapo kama lengo la mazoezi ya gym limetimia.

Baada ya wachezaji wote kuonekana wapo safi, Lwandamina ameamua kuwaongezea dozi ndogo kwa kufanya mazoezi asubuhi na jioni katika sehemu tofauti.

Kwa mujibu wa programu ya kocha, timu itaanza mazoezi ya viungo katika gym ya City Mall iliyopo Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam kabla ya jioni kufanya mazoezi Uwanja wa Uhuru, jijini kwa muda wa wiki nzima wakati wakifikiria sehemu ipi watakwenda kujichimbia kwa ajili ya kujinoa zaidi.

Msaidizi wa kitengo cha mawasiliano wa Yanga, Godlisten Chicharito, alisema programu hiyo ya kocha itaendelea hadi pale kocha Lwandamina atakapoamua kubadili kipindi ambacho tayari suala la wapi pa kwenda kuweka kambi litakuwa limejulikana.

“Hivi sasa tutafanya mazoezi asubuhi gym na jioni Uwanja wa Uhuru kwa muda wa wiki moja, baada ya hapo ndipo suala la kambi litakapowekwa wazi kwani hivi sasa uongozi upo kwenye kutatuta sehemu sahihi ya kwenda kujichimbia.

“Wapinzani wetu wamekwenda nje haitusumbui, kwani kipigo chao kipo palepale tunawasubiri wakirejea Dar es Salaam na kukutana nao kwenye mechi ya Ngao ya Jamii,” alisema.
Source: BINGWA

Comments

Popular posts from this blog

Kubemenda Mtoto

Siwezi pitisha siku bila kutembea na malaya

HAYA NDIO MADHARA YA KUFANYA MAPENZI KWA NJIA YA MDOMO. (Oral sex).