LWANDAMILA:Sasa mtaipenda YANGA

KOCHA Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, amesema program za mazoezi wanazozifanya wachezaji wake zitakifanya kikosi hicho kuwa imara na chenye kutoa ushindani katika kila mchezo watakaocheza msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao utaanza Agosti 26, mwaka huu.

Akizungumza na gazeti hili jana, Lwandamina alisema wachezaji wake watakuwa na nguvu na watafikia kiwango anachohitaji kwa sababu msimu huu amewapa mazoezi kuanzia mwanzo tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita ambapo alijiunga na timu hiyo katikati ya ligi.

Lwandamina alisema jukumu lake kubwa ni kuwapa wachezaji mbinu za kutawala mpira, kufunga, kuzuia kulingana na kila mpinzani anavyocheza.

"Ninatumaini nitakuwa na kikosi imara kutokana na maandalizi, nimeanza nao kuanzia awali, watapitia program zote muhimu nilizoziandaa ambazo zitawajenga na kuwaimarisha, watakuwa tofauti na mnavyowajua, naamini timu itakuwa ya ushindani kuanzia wenyewe kwa wenyewe," alisema Lwandamina.

Kocha huyo wa zamani wa Zesco ya Zambia, aliongeza kuwa licha ya baadhi ya wachezaji kuondoka katika kikosi hicho, hana wasiwasi na nyota waliosajiliwa huku wale aliokuwa nao walikuwa wameshaelewa falsafa zake.

"Utakuwa msimu bora pia, ninajua kazi yangu na wachezaji wanajua majukumu yao, sitaki kuzungumzia wachezaji walioondoka, ni lazima ukubali hali ya namna hii katika timu, ni jambo la kawaida, naamini hata klabu nyingine pia zimesajili wachezaji wapya ambao nao wanahitaji kujifunza na kujua mfumo wa timu," aliongeza Lwandamina.

Alisema kabla ya kukutana na Simba katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii Agosti 23, mwaka huu, anahitaji kikosi chake kipate mechi zisizopungua tano zikiwamo mbili na timu za nje ya Tanzania.

"Nataka kuona wachezaji wanapata changamoto kwa kucheza na timu zenye uwezo tofauti, hii itasaidia kujua walichokipokea katika mazoezi, najua ligi itakuwa ngumu kwa sababu kila klabu imejiimarisha," Lwandamina aliongeza.

Yanga inatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam kati ya kesho na keshokutwa kwenda Mbeya kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mbeya City ambayo pia inajiandaa na Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Mabingwa hao wa Bara ambao mwakani wataiwakilisha nchi katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wataanza kutetea ubingwa wao kwa kuikaribisha Lipuli FC ya Iringa inayofundishwa na Selemani Matola.

Comments

Popular posts from this blog

Kubemenda Mtoto

Siwezi pitisha siku bila kutembea na malaya