Mbeya:MADARASA MAWILI KUTUMIA CHUMBA KIMOJA
Wanafunzi wa shule ya msingi Magwalisi wilayani Mbarali mkoani Mbeya, wanatumia chumba kimoja, kwa wakati mmoja wakati wa kufundishwa wanafunzi wa madarasa wa ngazi tofauti kutokana na uchache wa vyumba vya madarasa,
Jonathan Chengula, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo amesema kuwa shule yao ina vyumba vinne tu vya madarasa, hali ambayo inawapa ugumu wakati wa ufundishaji wa wanafunzi.
“Tungeweza kuchangiwa na wazazi tukaongeza madarasa hata hivyo, shule ipo kwenye mgogo na inadaiwa kuwa ndani ya mipaka ya Mamlaka ya Hifadi ya Taifa (TANAPA), hivyo wazazi wanahofia kuongeza vyumba vya madarasa kisha shule ije kuhamishwa,” amesema Chengula.
Wema Amosi, mwanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo, amesema; “Tunaiomba serikali ituongezee majengo mengine ili tuweze kumudu masomo ambayo tunafundishwa darasani, tukiongezewa vyumba vya madarasa itakuwa msaada mkubwa kwetu.”
Clemencia Kitalima, mwanafunzi mwingine wa darasa la sita, amesema uchache wa vyumba vya madarasa umekuwa ukipelekea chumba kimoja kusomea wanafunzi wa madarasa mawili hali ambayo inaawathiri wanafunzi hao kutokana na kutosoma kwa nafasi.
“Tunaingia chumba kimoja ingawa sisi ni madarasa mawili tofauti kwahiyo tunageuziana migongo na walimu wawili tofauti wanatufundisha,” amesema.
Goden Mgombavanu, mwenyekiti wa kitongoji cha Nyalunga, ilipo shule hiyo amemwambia mwandishi wa habari hii kuwa, changamoto kubwa iliyopo ni mgogoro wa mipaka ya Tanapa, hivyo kushindwa kuendelea na ujenzi kwa hofu ya kuja kuhamishwa.
“Ni kweli, shule hii ina vyumba vichache na watoto wetu wanateseka hivyo ni vema serikali ikaliona hili ili mipaka halisi ya shule uweze kufahamika na wazazi waweze kuendelea na ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa gharama zao,” amesema Mgombavanu
Comments
Post a Comment