MAUAJI KIBITI YAMWAGA MACHOZI ACT-WAZALENDO
Chama cha ACT Wazalendo kinasikitishwa na taarifa za mauaji yanavyoendelea Mkoa wa Pwani katika eneo la MKIRU (Mkuranga, Kibiti na Rufiji), hasa baada ya taarifa ya mauaji ya watu wawili yaliyotokea usiku.
Kiongozi wa Chama Cha ACT Wazalendo Ndugu Zitto Kabwe ameonyesha masikitiko yake kwa kueleza yafuatayo, "Tunahitaji kushikamana Kama nchi kwenye suala la MKIRU. Mauaji yanayoendelea huko hayapaswi kupewa nafasi kuendelea. Taifa lizungumze lugha moja kukabiliana na hali Hii. Ninarejea wito niliotoa siku zilizopita kuwa ninatarajia Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama itakwenda Eneo la MKIRU kuzungumza na wananchi wa kule ili kupata maarifa ya kuishauri na kuisimamia Serikali kudhibiti mambo na kuimarisha usalama". Mwisho wa kunukuu.
ACT Wazalendo tunaungana na wananchi wote na wapenda amani nchini Tanzania kulaani vikali mauaji hayo. Tunayaona mauaji hayo kama tishio na jaribio juu ya uhuru wetu na usalama wa taifa letu, mambo ambayo yanatuunganisha wote bila kujali itikadi, dini, hali ya kiuchumi wala rangi. Hatuamini kwa namna yoyote kuwa wauaji hao ni watu wenye nia njema wala agenda ambayo njia pekee ya kuifikia ni kupitia mauaji ya watanzania wenzao. Hawa ni wahalifu na wanaostahili nguvu ya umoja wetu dhidi ya udhalimu wao.
Tunamshauri Rais aitishe Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa, na kufanya maazimio muhimu ya kukabiliana na halii hii ya kipekee kutokea katika nchi yetu.
Tunaviomba vyombo vya ulinzi na usalama kushirikiana na wananchi kutokomeza mauaji haya na wadhalimu hao. Tunavitia moyo vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, viongozi wao, pamoja na askari wetu wote kutorudi nyuma hadi hali ya utulivu na usalama irejee kama awali.
Pamoja na hayo, ni muhimu vyombo vya ulinzi na usalama navyo vishiriki kujenga umoja wa wananchi katika wakati huu mgumu kwa Taifa kwa kutenda haki kwa wananchi wa maeneo haya bila kuonekana vinafanya uonevu. Tunapinga kamata kamata inayoendelea dhidi ya viongozi na wanachama wa Chama cha Wananchi, CUF katika eneo la MKIRU, bila maelezo ya kutosha, hilo ni moja ya mambo yanayoondoa umoja wetu katika wakati huu tuliopaswa kusimama pamoja.
Mwisho, tunapenda kuwakumbusha Watanzania wote kuwa kwa mujibu wa Katiba yetu, jukumu la ulinzi na usalama wa nchi ni la kila mwananchi na haswa kila mzalendo. Huu ni wakati wa kuonyesha uzalendo wetu. Huu ni wakati ambapo Taifa letu linatuita. Shime kila mmoja wetu kwa nafasi aliyonayo na kwa taarifa alizonazo zinazoweza kusaidia kupatikana kwa watu hawa na ashirikiane na vyombo vya ulinzi na usalama ili kusaidia kurudisha amani yetu.
Nchi Kwanza, Taifa Kwanza, Usalama Kwanza! Leo na Kesho
Comments
Post a Comment