Kituo cha polisi kilicho telekezwa kwa miaka mingi


Picha ya mtandao

Mwanza. Wakati vijiji, kata na maeneo mbalimbali hapa nchini wananchi wakichangishana fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya polisi ili kuimarisha ulinzi na usalama, hali ni tofauti katika Kata ya Nyegezi ambako kituo kilichoanzishwa miaka 10 iliyopita hakijakamilika. 

Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki, Kaimu Mtendaji wa kata ya hiyo, Jonas Mugisha alisema baada ya kituo hicho kilichofikia hatua ya linta kushindwa kukamilika kwa wakati, wapo kwenye mipango ya kuishirikisha jamii kuchangia ujenzi ili kusaidia usalama wa wakazi na abiria wanaotumia eneo hilo. 

Alisema kata hiyo yenye mitaa minane ina zaidi ya kaya 3,000 zikiwa na wakazi 20,955 kati yao wanawake ni zaidi ya 11,000 na wanaume zaidi ya 9,000. 

Mitaa hiyo na idadi ya wakazi katika mabano ni Nchenga (2,250), Kalfonia (3,165), Nkamba (2,532), Nyabulogoya (1,962), Swila (2,231), Ibanda (3,409), Kuzenza (2,094) na Igubinya (1,780). 

“Hili jambo na sisi tumekwishalijadili ila kwa sasa tunataka kuwashirikisha wananchi maana kwa maelekezo maana wananchi wanatakiwa kushiriki shughuli hii ili Serikali imalizie,” alisema kaimu mtendaji huyo na kuongeza: 

“Tunaendelea na vikao vya kamati za ndani kupanga mipango ya namna ya kumalizia ujenzi na baada ya hapo tutaitisha mikutano ya hadhara ili kuwafahamisha wananchi kushiriki kuchangia ili kumaliza ukamilishwaji wa kituo hicho.” 

Wadau wazungumza 

Mwenyekiti wa Stendi ya Mabasi Nyegezi, Peter Maroro alisema inahudumia zaidi ya watu 18,000 kwa siku wanaoingia na kutoka jijini Mwanza. 

Maroro alisema stendi hiyo ina wafanyabiashara zaidi ya 1,500 ambao ni wakala wa mabasi, mamalishe, wamachinga, wauza samaki na wale wa mbogamboga. 

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nchenga ilipo stendi na kituo hicho, Paschal Joseph alisema ujenzi wake ulianza wakati ikiwa ni Kata ya Butimba na kwamba, usalama wa eneo hilo unasaidiwa na uongozi mpya wa stendi ulioweka mikakati madhubuti ya kulinda eneo hilo. 

“Ni kweli ukiangalia mzigo huu tunaoubeba tunatakiwa kuwa na usalama zaidi ya hapa, lakini sisi kama mtaa hatuna fungu la kujenga kituo cha polisi badala yake huwa tunapendekeza mambo ambayo tunayaona ni ya muhimu na kuyawasilisha kwenye uongozi wa kata. 

Hata hivyo, anasema atafuatilia zaidi suala hilo polisi kujua mipango iliyopo. 

Jitihada za kuimarisha ulinzi 

Akizungumzia suala la kuimarisha usalama, Mwenyekiti wa Stendi ya Mabasi Nyegezi, Maroro anasema kutokana na vitendo vilivyokuwa vimekithiri vikiwamo vya uhalifu, uvutaji bangi na unywaji wa viroba walilazimika kufanya mabadiliko ya uongozi ili kutengeneza mfumo mpya kituoni hapo. 

Miongoni mwa mabadiliko ni pamoja na kuunda kamati mbili; moja ikiwa ya maadili yenye watu 18 na ya ulinzi na usalama yenye wajumbe 33 ambayo hufanya kazi kwa muda wa saa 24 kwa kujitolea, lengo likiwa kuimarisha usalama wa eneo hili. 

Katika kuhakikisha suala hilo linafuatwa, viongozi wameweka adhabu na kanuni ambazo mtu anapokiuka utaratibu huo hupewa onyo, kulipa faini ya Sh30,000 na kuondolewa kituoni kwa muda wa wiki mbili. 

Kwa mujibu wa Maroro, uongozi huo umezungumza na wamiliki wa mabasi wakiwataka wawape wanaohusika na shughuli za ukataji tiketi namba maalumu za utambuzi. 

Maroro anasema katika kuboresha jambo hilo, uongozi wao umeweka utaratibu wa kila kibarua anayekata tiketi kuhakikisha anavaa sare yenye namba na jina la kampuni anayokatia tiketi ili kutambulika kwa urahisi. 

“Baada ya kuanzisha utaratibu huu Machi, ililazimika tuanze kazi ya kutambuana kati ya watu 187 waliotakiwa kutambuliwa na 107 walifukuzwa kutokana na tabia na vitendo vyao, hivyo kubaki na watu 80,” alisema Maroro. 

Hata hivyo, anasema baada ya kumaliza utambuzi walilazimika kuendesha operesheni iliyofanywa katika maeneo mbalimbali yanayozunguka stendi hiyo, ambapo vijana wengine 50 walibainika kutumia bangi, ulevi, kukutwa na visu nyembe na vifaa vingine vya kuhatarisha maisha ambapo 31 walipelekwa mahakamani na wengine kuondolewa. 

Diwani wa Nyegezi, Edith Mudogo anasema anafanya utaratibu wa kutafuta wafadhili watakaosaidia kukimalizia kituo hicho cha polisi. 

Anasema bila kufanya hivyo inaweza kuchukua muda mwingine zaidi kukikamilisha. 

Mmoja wa askari wanaofanya kazi katika kituo kidogo cha polisi kilichopo kwennye stendi hiyo aliyeomba hifadhi ya jina lake, anasema yapo matukio yanayofanywa ambayo yanahatarisha usalama wa maisha ya binadamu na wao (askari) ni wachache kulinganisha na idadi ya wananchi. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi anasema ukata ndiyo umesababisha ujenzi wa kituo hicho ukwame licha ya kudai kuwa wapo kwenye mchakato wa kutafuta wadau kuwasaidia kukikamilisha. 

Kata ya Nyegenzi ndipo ilipo stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani ambayo ilihamishiwa tangu mwaka 2007 kutoka katikati ya jiji eneo la Tanganyika, lengo likiwa ni kuipanua na pia ilipokuwa kutotosheleza mahitaji kutokana na udogo. 

Source: Mwananchi

Comments

Popular posts from this blog

Kubemenda Mtoto

Siwezi pitisha siku bila kutembea na malaya