Maiti zaokotwa



MAITI tatu zimeokotwa kwenye fukwe mbalimbali za Zanzibar katika siku tatu zilizopita zikiwa zimeharibika vibaya, kuwa na majeraha ya kukatwa na kitu chenye makali zikiwa zimefungwa kwenye viroba. 


Maiti ya mwisho iliokotwa jana katika ufukwe wa bahari wa Mtende, Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa na majeraha na kufungwa katika kiroba. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Juma Sadi, aliiambia Nipashe mwili huo ulikuwa umeharibika vibaya hivyo kulazimika kuzikwa katika eneo hilo, kutokana na kutotambuliwa wala kuwa na nyaraka ama taarifa zozote za kuitambua maiti yake. 

Alisema mwili huo uliokotwa majira ya saa mbili asubuhi jana na wakazi wa eneo hilo ambao wanadhani kuwa ulisukumwa na wimbi la maji ya bahari kutoka eneo la mbali. 

Alisema hiyo ni maiti ya tatu kukutwa katika fukwe za bahari katika mkoa huo katika siku tatu, baada ya mwili wa kwanza kuokotwa Jumatatu katika pwani ya Bungi na nyingine kukutwa katika ufukwe wa bahari ya Makunduchi juzi. 

“Maiti zote tatu zilizokutwa katika fukwe ya bahari katika mkoa huu na moja iliyokutwa Jumapili katika fukwe ya bahari Fumba, mkoa wa Mjini Magharibi, zimejeruhiwa kwa kukatwa viungo vya mwili na kutiwa katika viroba,” alisema Kamanda Sadi. 

Alisema maiti hizo zote ziliharibika na kulazimika kuzikwa katika eneo la ufukwe wa bahari; katika maeneo ilikookotwa. 

Alisema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi ili kupata taarifa kama kuna mtu aliyepotea ili kuhusisha na matukio hayo yanayofanana. 

Aidha, Kamanda Sadi aliitaka jamii kusaidia kutoa taarifa ya kupotelewa na jamaa au ndugu zao ili kulisaidia jeshi hilo kuharakisha upelelezi juu ya maiti hizo ambazo ni za wanaume wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35 hadi 40. 

Akizungumzia maiti hizo, Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja, Idrisa Kitwana, alisema matukio hayo siyo ya kawaida katika wilaya hiyo kwa kuwa yanafanana. 
Alisema miili hiyo yote ilikutwa katika fukwe hizo za bahari ikiwa imekatwa mikono na miguu na kufungwa katika viroba. 

“Inaonekana maiti hizi zimeuliwa na kutupwa baharini na tuna wasiwasi kuwa sio za maeneo ya karibu ya Zanzibar," alisema Kitwana. 

"Tunataka kuwasiliana na wenzetu wa Tanzania Bara maana kuna matukio mengi ya mauaji; hasa huko Kibiti mauaji yameshika kasi.” 

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz, aliiambia Nipashe jana kuwa uchunguzi bado haujathibitisha kama miili hiyo inatoka Kibiti. 

KUOANISHA MIILI 
Kamanda Boaz alisema ni vigumu kuoanisha miili hiyo na matukio yanayoendelea kutokea katika mkoa wa Pwani ambako wauaji wamekuwa wakiondoka na miili ya baadhi ya watu wanaowaua. 

Alisema kwa kuwa miili ya Zanzibar imeonekana ufukweni, ni vigumu kufahamu wapi ilikotokea. 

“Kama unakumbuka ilitokea ajali ya ndege kwenye nchi za wenzetu (Malaysia), lakini baadaye moja ya mabaki (ya ndege hiyo) yalionekana Zanzibar,” alisema Kamishna Boaz. 

“Ndiyo maana miili hii ni vigumu kujua kwa sasa chanzo chake ni wapi mpaka upelelezi ukakamilike,” alisema. 
Matukio ya Zanzibar ni mara ya pili kwa maiti nyingi kukutwa kwenye viroba wakati mmoja. 

Kati ya Desemba 6 na 8 mwaka jana, maiti saba ambazo hazikutambulika zilikutwa zikielea katika Mto Ruvu, Bagamoyo mkoani Pwani, zikiwa pia zimehifadhiwa kwenye viroba na kuharibika vibaya. 

Diwani wa Kata ya Makurunge, Paul Kabile aliviambia vyombo vya habari wakati huo maiti hizo zilikuwa za jinsia ya kiume na ziligunduliwa na wavuvi. 

Alisema maiti hizo kila moja ilikuwa imehifadhiwa kwenye kiroba huku zikiwa zimewekewa mawe na mifuko hiyo kushonwa juu kama iliyohifadhiwa nafaka. 

Miezi sita iliyopita serikali ilisema inaendelea na uchunguzi juu ya maiti hizo, na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akazihusisha na wahamiaji haramu ambao husafirishwa katika mazingira mabaya. 

Mwigulu alitolea mfano wa gari lililokamatwa na wahamiaji haramu 81 wakiwa kwenye hali mbaya na kusema huenda maiti hizo zinatokana na wahamiaji haramu kama hao

Comments

Popular posts from this blog

Kubemenda Mtoto

Siwezi pitisha siku bila kutembea na malaya