Walimu waliojikuta wamelala nje na kunyolewa wageuziwa kibao
- Get link
- X
- Other Apps
Buchosa. Wananchi wa Kisiwa cha Soswa halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema wamewatupia mpira walimu waliojikuta wamelala nje kwa madai ya imani za kishirikina kuwa ni tukio la kutengenezwa.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa jana Alhamisi kwa dharura kujadili suala hilo lililojitokeza usiku wa kuamkia Novemba 15, mwaka huu, katika viwanja vya shule ya msingi Soswa wananchi hao walisema tukio hilo ni la kutengenzwa ili kuishinikiza Serikali iwape uhamisho kutokana na mazingira magumu wanayokaa.
Mzee wa kisiwa hicho, Mashinga Boniphace (80) alisema hakuna ukweli juu ya tukio hilo kwani yeye pamoja na wazee wenzake waliangalia vibuyu na damu iliyokuwa imetapakaa ndani ya nyumba za walimu hao sio ya kishirikina.
“Walimu hao waliamua kuua ndege aina ya nyagenyange ili na kutapakaza damu hizo ndani ya nyumba zao pamoja na kwenye vibuyu ili kushinikiza uongozi wa juu kuwahamisha kutokana na juhudi zao za kuhama kugonga mwamba,”alisema Boniphance
Kauli ya mzee huyo wa mila ilipingwa na mkazi mwingine wa kijiji hicho, Mjula Magafu ambaye alisema suala hilo liangaliwe kwa kina kwakuwa limezua sintofahamu ndani ya kisiwa hicho na Taifa kwa ujumla.
Alisema kama walimu ndio walitengeneza tukio hilo wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa kudanganya umma.
Soma: Spika ataka Serikali kutoa majibu kuhusu walimu kukutwa wamelala nje
“Hapo awali lilipotokea tukio la nyumba zao kupondwa mawe walimu wote waliondoka na kubaki wawili ambapo hakukuwa na kitendo kama hicho, baadaye walimu waliokuwa wamesusia akiwemo mwalimu Daudi Shule na Wape Kisimu kitendo hicho kilijirudia tena na sasa wameamua kutengeneza tukio la kulazwa nje, tunapaswa kuchunguza kwa kina,” alisema Magafu
Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na Mwananchi walisema tukio hilo limewaathiri kimasomo hivyo kushindwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao.
Mwanafunzi wa darasa la tano, Malisela James aliiomba jamii ikubali kuwa walimu hao wamefanyiwa vitendo vya kishirikina na kwamba watafute namna ya kukukomesha ili kuwapa fursa ya kuendelea kusoma.
Mwenyekiti wa kamati ya shule, Lidia Buluba alilaani kitendo hicho ambacho kinahisishwa na imani za kishirikina huku akiwatupia lawama baadhi ya walimu waliotengeneza jambo hilo ili wapatiwe uhamisho kwa madai kuwa mazingira wanayoishi si mazuri.
Mwalimu Daudi Shule ambaye anapatiwa matibabu ya asili katika kijiji cha mwangakia yeye alidai alinyolewa sehemu za siri, mwalimu Ernest Katunzi alithibisha kwa kumwona sehemu hizo kuwa amenyolewa pamoja na mwalimu Wape Kisumo aliyonyolewa nywele kichwani kwa pamoja walisema kuwa wanafanyiwa vitendo vya kishirikina hata kipindi wanapondwa mawe jamii hiyo haikuamini.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Petro Lukas alisema maneno yanayosemwa na jamii hawawezi kuyaamini na haamini kama walimu wametengeneza mazingira ya tukio hilo ili wahame kwa kuwa kazi yao ni kufundisha.
Mtendaji wa Kata ya Bulyaheke, Musa Mwilomba alisema kuwa anaiomba jamii kutokutupiana mpira juu ya tukio hilo na kwamba wanatakiwa kusameheana na kusahau kilichotokea ili kuanza sura mpya na walimu waendelee kufundisha.
Mkaguzi wa shule wilayani Sengerema, Elly Msulu aliyefika katika Kisiwa cha Soswa kupata ukweli juu ya tukio hilo aliitaka uchunguzi zaidi ufanyike kujua ukweli wa tukio hilo na watakaobainika hatua kali za kisheria dhidi yao zitachukuliwa huku akiwaomba walimu kuwa wavumilivu wakati suala hilo linatafutiwa ufumbuzi
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment