Dr Slaa Aajiriwa Kwenye Duka la SuperMarket Canada


Aliyekuwa  Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, ameajiriwa katika duka kubwa la bidhaa za majumbani (Supermarket) la Costco lililopo Oakville, Toronto nchini Canada, imebainika.

Dk. Slaa, kwa sasa anaishi nchini Canada alikokwenda kwa masomo, tangu alipotangaza kuachana na siasa Septemba 1, mwaka 2015.

Kwa muda wa wiki kadhaa, ziliibuka taarifa katika mitandao ya kijamii kuwa mbunge huyo wa zamani wa Karatu, amemaliza masomo yake na sasa anafanya kazi katika moja ya maduka makubwa ya bidhaa mbalimbali nchini humo – Supermarket.

Supermarket ya Costco anayofanya kazi Dk. Slaa akihudumu kama Mshauri wa Mauzo (Sales Advisor), akilipwa Dola za Marekani 10 (zaidi ya Sh 20,000) kwa saa, ina hadhi kama Nakumat, Shopers, Imalaseko, Game na maduka mengine makubwa nchini.

Akizungumza na Gazeti la Mtanzania jana kwa simu , Dk. Slaa alisema kuwa kwa sasa anaishi kwa kazi ya mikono yake  kwani ili aweze kuishi anahitaji kufanya kazi zaidi ya mbili hadi nne kwa siku.

“Niko, ninafuatilia matukio Mutukula (ziara ya Rais Dk. John Magufuli jana). Siku zote nimesema ninaishi kwa jasho na kazi ya mikono yangu. Canada ili uishi vizuri, unahitaji kazi zaidi ya mbili au tatu mpaka nne. Hayo nimeweka wazi, sijui jambo jipya kama mtu alikuwa hafuatilii.

“Mimi ninafanya kazi PWD/CDS/COSTCO kama Sales Advisor, baada ya kumaliza masomo yangu hasa Interpersonal Communication. Costco ninakofanya kazi ina members (wanachama) 10,000.  Kwa siku wanaofika Warehouse ni kati ya 5,000 hadi 7,000,” alisema Dk. Slaa.

Mbali na hilo, alisema kuwa pia anafanya kazi nyingine ikiwa ni pamoja na ushauri (Consultancy).

Alisema kila mara amekuwa akiwataka Watanzania na vijana wafanye kazi kwani fedha haziji kwa kukesha kwenye mtandao wala propaganda.

“Canada ni kazi, Profesa wa Chuo Kikuu anafanya kazi ya Uber. Sijui kama Uber inafahamika Tanzania, ni dereva Taxi kwa kutumia gari lake binafsi. Ofisa wa Serikali usiku anaosha vyombo hotelini.

“Ndiyo maana familia ina magari mawili au zaidi, TV, nyumba ya kisasa, chakula cha kisasa. Wanatekeleza sera ya ‘Hapa Kazi Tu’ kwa matendo. Nadhani nimekupa taarifa za kutosha ikiwa ni pamoja na kujibu propaganda kuwa nilihongwa mabilioni.

“Niwahakikishie tena, wakati wa kusoma nilikuwa na scholarship, tangu nianze kazi ninaishi kwa jasho la mikono yangu. Mke wangu yeye ameingia Chuo Kikuu cha York baada ya Diploma yake na bado anapata scholarship.

“Ndiyo maana tuna uwezo wa kuwa na magari mawili aina ya Jeep na Dodge, ukifanya kazi utaishi vizuri. Hii ni pamoja na kugharamiwa bima ya afya (Health Insurance), watoto kusomeshwa na Serikali ya Canada,” alisema Dk. Slaa.

Mei mwaka huu, Dk. Slaa, alisema hana mpango wa kurudi nchini kwa sasa na kwamba taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii hazina ukweli wowote.

Hata hivyo, Dk. Slaa ambaye alipata kuwa Mbunge wa Karatu kwa vipindi vitatu mfululizo, hakuweza kuainisha mazingira yaliyomfanya aondoke nchini na kwenda kuishi ughaibuni.

Septemba, 2015 wakati wa Uchaguzi Mkuu, Dk. Slaa alijiweka kando na siasa, kwa kile alichokieleza kutofautiana na viongozi wenzake ndani ya chama chake juu ya masharti ya kumpokea aliyekuwa mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.

“Sina tabia ya kuyumbishwaa, sina chuki na mtu yeyote, sipendi siasa za udanganyifu na propaganda. Nimeachana na siasa tangu Julai 28, 2015, baada ya kuona misingi ya chama nilichoshiriki kukijenga imepotoshwa,” alisema Dk. Slaa siku alipotangaza kuachana na siasa.

Alisema sharti la kwanza ambalo alitaka Chadema izingatie, ni kiongozi huyo wa zamani ndani ya Serikali ya CCM, kujisafisha dhidi ya tuhuma ya kashfa ya sakata la Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond aliyohusishwa nayo akiwa Waziri Mkuu.

Credit: Mtanzania 

Comments

Popular posts from this blog

Kubemenda Mtoto

Siwezi pitisha siku bila kutembea na malaya