Hizi ndizo sababu za Ngoma kusepa YANGA



MSHAMBULIAJI WA TIMU YA YANGA, DONALD NGOMA

HUKU mshambuliaji wa kimataifa wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, Donald Ngoma, akiwa nje ya kikosi cha timu hiyo kutokana na kuelezwa kuwa ni majeruhi wa goti, imebainika kuwa sababu ni kutokana na kuidai klabu hiyo fedha za usajili.

Akizungumza na Nipashe mmoja wa watu wa karibu na Ngoma (jina tunalihifadhi), alisema Ngoma ni mzima na kwamba yupo katika "mgomo baridi" wa kuitumikia Yanga ambayo inadhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, akishinikiza kulipwa kwanza fedha zake za usajili kama walivyokubaliana.

Chanzo hicho kilisema kuwa kutokana na Yanga kushindwa kutimiza makubaliano hayo licha ya Ngoma kusaini mkataba wa miaka miwili, mshambuliaji huyo amesema kuwa tayari mkataba waliosaini umevunjika rasmi.

Aliongeza kuwa kutokulipwa kwa fedha hizo, kumemfanya mshambuliaji huyo kuchukua uamuzi wa kujiweka pembeni kwa sababu hapati majibu ya kueleweka kuhusiana na madai yake.

"Sababu kubwa ya Ngoma kuikacha Yanga ni kuwa anawadai, anasema wanamzungusha, hilo ndiyo tatizo kuu na si majeruhi kama ilivyokuwa hapo awali, anajuta kwa nini alisaini mkataba mpya ambao bado hajafaidika nao kama walivyokubaliana," kilisema chanzo hicho.

Katibu Mkuu wa Yanga , Boniface Mkwasa, aliliambia gazeti hili jana kuwa wamemwandikia mshambuliaji huyo barua mara mbili za kujieleza, lakini bado hajatoa majibu yoyote kuhusiana na hatua ya kuondoka nchini bila kupewa ruhusa na klabu.

Hata hivyo, Mkwasa, kocha wa zamani wa mabingwa hao watetezi hakuwa tayari kuweka wazi kama Ngoma anaidai au haidai Yanga na kusema kuwa mshambuliaji huyo ni mali yao.

Mkwasa alisema kuwa Ngoma ni mchezaji halali wa Yanga ambaye alisaini mkataba wa miaka miwili Julai mwaka huu na endapo ataendelea kukaa nje ya kikosi, hatua kali dhidi yake zitachukuliwa ili iwe fundisho kwa wachezaji wengine kutofanya kosa kama hilo.

"Kwanza tulikuwa hatujui yuko wapi, tukamwandikia barua kupitia barua pepe ajieleze yuko wapi, hakuijibu, baadaye kupitia mitandao tunaona yuko Zimbabwe, tukamtumia barua nyingine ili aseme kwa nini ameondoka nchini bila ruhusa, amekaa kimya hadi leo (jana), sasa tunashangaa kuona ameitwa katika timu ya Taifa, wamemuona wapi wakati yeye ni majeruhi?" Alihoji Mkwasa.

Katibu huyo aliongeza pia wamefurahishwa na uteuzi alioupata, lakini wanashangaa kusikia mshambuliaji huyo ni mchezaji huru, jambo ambalo si la kweli na klabu yake inafahamu wazi ana mkataba ambao unambana na anatakiwa kuitumikia timu kwenye mechi za ligi na mashindano mengine watakayoshiriki.

Source: Nipashe

Comments

Popular posts from this blog

Kubemenda Mtoto

Siwezi pitisha siku bila kutembea na malaya

HAYA NDIO MADHARA YA KUFANYA MAPENZI KWA NJIA YA MDOMO. (Oral sex).