Hamisa Mobeto Adaiwa Kumfanyia Mwanae Aliyezaa na Diamond Ukatili


SIKU chache baada ya kutoswa malezi ya mwanaye, Abdul Nasibu ‘Prince Abdul’ ambapo alimfungulia kesi mahakamani ya madai ya malezi mzazi mwenziye ambaye ni msanii wa Bongo Fleva, lakini Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar, upande wa Watoto ukatupilia mbali shitaka hilo, mwanamitindo maarufu Bongo, Hamisa Hassan Mobeto anadaiwa kumfanyia ukatili mwanaye huyo.



TUJIUNGE NA CHANZO

Chanzo makini kilicho karibu na familia ya Mobeto kililimwagia ubuyu Ijumaa Wikienda kuwa, mrembo huyo, licha ya kuwa mtoto wake bado mdogo ana umri wa miezi minne, amekuwa akimtelekezea mama’ke mzazi, Shufaa Lutigunga na kusafiri mara kwa mara nje ya nchi.

“Yaani kwa kweli inatushangaza sana, kweli mtoto ana umri wa miezi minne, unaanzaje kumuacha na kwenda mbali kiasi hicho? “Mara utasikia leo yupo Nairobi, mara utasikia yupo Dubai sasa hapo unategemea nini?,” kilimwaga ubuyu chanzo hicho.

CHANZO CHAZIDI KUTIRIRIKA

Chanzo hicho makini kiliendelea kutiririka kuwa, Mobeto tangu ajifungue, amekuwa akisafiri mno na kumwacha mtoto, jambo ambalo linawapa maswali watu wengi kwamba, ina maana hamnyonyeshi hivyo
anaweza kumfanya mtoto adumae kwani maziwa ya mama ni muhimu kwa mtoto mchanga katika miezi sita ya kwanza.

“Kila mtu anafahamu umuhimu wa maziwa ya mama kwa mtoto mchanga hususan katika kipindi cha miezi sita ya awali, tunatilia shaka sana anaweza hata kumbemenda mtoto maana hatujui kule anaenda kukutana na wanaume tofauti, akishiriki nao je?” Kilihoji chanzo hicho.

NI SIKIO LA KUFA?

Chanzo kiliendelea kutiririka kwamba huenda Mobeto ni sikio la kufa kutokana na mambo anayoyafanya kwani kwa mtu mwingine alivyoshambuliwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu suala la kuzaa na Mbongo Fleva ambaye anajua kabisa yupo kwenye uhusiano na Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, pamoja na kuanika picha zao wakiwa faragha, hakukoma, bado anaendelea tu na mambo hayo.

“Hamisa (Mobeto) ni sikio la kufa maana kuna habari kwamba juzikati alikuwa Dubai alikokwenda kujirusha na huyo baba mtoto wake wakati ameshamtosa kwenye malezi ya mtoto. “Kwa mtu ambaye anasikia asingekubali kwenda kujirusha na mtu wa hivyo. “Kuna picha ambazo zimesambaa akiwa amepiga na mrembo mmoja huko Dubai ambapo mrembo huyohuyo
ameonekana akiwa amepiga picha na msanii huyo wa Bongo Fleva, jambo ambalo linaashiria walikuwa pamoja,” kilidai chanzo hicho.

MOBETO ANASEMAJE?

Ili kuujua ukweli wa habari hizo, Ijumaa Wikienda kama ilivyo desturi yake ya kupata mzani (balance), lilimtafuta Mobeto ambapo mazungumzo yalikuwa hivi;
Ijumaa Wikienda: Habari yako, ninaongea na Mobeto?

Mobeto: Ndiyo, nani mwenzangu?
Ijumaa Wikienda: Unaongea na Gazeti la Ijumaa Wikienda hapa.
Mobeto: Okey, sema…
Ijumaa Wikienda: Kuna habari kwamba umekuwa ukimtelekezea mama yako mtoto na kusafiri mara kwa mara na juzi tu ulikuwa Dubai ulikokwenda kujirusha na baba mtoto wako, msanii wa Bongo Fleva, unazungumziaje?
Mobeto: No coment…. (akakata simu).

KUTOKA KWA MHARIRI Ni vyema Mobeto akawa makini na suala la malezi kwani kwa kawaida, katika miezi sita ya awali, mtoto anahitaji zaidi maziwa na malezi ya ukaribu ya mama na baba licha ya kwamba baba mtoto anadaiwa kugomea malezi, kinyume na hapo ni ukatili mkubwa kwa mwanaye huyo.

Comments

Popular posts from this blog

Kubemenda Mtoto

Siwezi pitisha siku bila kutembea na malaya