YANGA YATOA PIGO SIMBA

MMOJA WA WACHEZAJI WA TIMU YA SIMBA, JUUKO MURSHEED ANAYEWANIWA NA TIMU YA YANGA

KAMA mazungumzo yanayoendelea kati ya uongozi wa klabu ya Yanga na wachezaji wawili wa klabu ya Simba yatakamilika, Wanajangwani hao kwa mara ya nyingine watakuwa wametoa pigo kwa vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa kama ilivyo kwa Simba na Singida United,  ipo kwenye mazungumzo ya siri na kiungo Muzamir Yassin na beki wa kati raia wa Uganda, Juuko Mursheed, ikijaribu kuwashawishi kutua kwenye timu hiyo katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.

Yanga imetuma wajumbe wake wa kamati ya usajili jijini Nairobi inapofanyika michuano ya Kombe la Chalenji, kufanya mazungumzo na nyota hao.

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alimwambia mwandishi wetu kuwa, kwa upande wa Muzamir mazungumzo ya awali yanatoa ishara ya mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar kuweza kutua kwenye kikosi chao hivi karibuni.

"Kuhusu Juuko, bado wapo kwenye mazungumzo, nafikiri baada ya siku chache lolote linaweza likatokea... wachezaji hawa wawili, kimkataba wanaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine kwa sababu mikataba yao imebaki miezi sita kumalizika," alisema Mjumbe huyo.

Aidha, taarifa zilieleza kuwa wachezaji hao wanasakwa vilivyo na Yanga kwa ajili ya kwenda kuchukua nafasi za kiungo Thaba Kamusoko ambaye ni majeruhi pamoja na beki Vincent Bossou aliyeamua kuachana na Yanga.

Muzamir yupo kwenye kikosi cha Kilimanjaro Stars kwenye michuano hiyo ya Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), huku Juuko akiwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda 'The Crane'.

Comments

Popular posts from this blog

Kubemenda Mtoto

Siwezi pitisha siku bila kutembea na malaya