HAJI MWINYI AZUNGUMZIA MUSTAKABALI WAKE NDANI YA YANGA
Baada ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Chalenji, beki wa kushoto wa Yanga, Haji Mwinyi amefunguka kuwa kama ataendelea kuwekwa benchi kwenye timu hiyo atakuwa tayari kuandika barua ya kuomba kuachwa.
Beki huyo alionyesha uwezo wa hali ya juu kwenye michuano hiyo iliyomalizika hivi karibuni nchini Kenya akiiwakilisha Zanzibar Heroes ambapo timu yake ilimaliza nafasi ya pili.
Licha ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo, lakini nafasi yake ndani ya Yanga ni finyu huku akiwekwa benchi na Gadiel Michael.
Mwinyi alisema kuwa kwa sasa anaona nafasi yake ya kucheza kwenye timu hiyo ipo wazi kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa.
“Nashukuru Mungu kwa kuweza kufanya vizuri kwenye michuano ya Chalenji, ukweli siyo kwamba nimeisha isipokuwa tu kuna mambo madogomadogo ndiyo yalikuwa yanatatiza kwa upande wangu lakini kila mmoja ameona nilichokifanya Kenya.
“Najua Gadiel Michael ni mchezaji mzuri amenipa changamoto kubwa na naamini nafasi yangu ya kucheza ipo wazi katika kipindi hiki labda yatokee mambo mengine ila kocha akinipa nafasi kila mmoja atafurahia kazi yangu hasa mashabiki wetu wa Yanga na kama itashindikana basi nitaomba niachwe ili niweze kwenda sehemu itakayopata nafasi ya kucheza," alisema Mwinyi.
SOURCE: CHAMPIONI
Comments
Post a Comment