YANGA KULAMBA DUME KUTOKA KWA DANGOTE


MICHAEL MAURUS NA HUSSEIN OMAR

YANGA wanaweza kulamba dume kwa mfanyabiashara Alhaji Aliko Dangote, katika mpango wao wa kumtaka kununua hisa asilimia 49 za klabu yao ili kuifanya kutoka katika mfumo wa uendeshaji wa wanachama na kuhamia ule wa kampuni.

Imeripotiwa kuwa Yanga ipo katika mkakati wa kumshawishi Dangote kununua hisa za Kampuni ya Yanga ili kuiwezesha klabu hiyo kujiendesha kisasa zaidi kama ilivyo Manchester City ya England na klabu kadhaa nyinginezo barani Ulaya.

Hilo linakuja siku chache baada ya Simba kuhama kutoka katika mfumo wa uendeshaji wa timu wa wanachama na kuwa wa uuzaji hisa, ambapo mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’, ndiye aliyetangazwa kushinda zabuni hiyo.

Mo alikidhi vigezo vyote vilivyoainishwa na kamati iliyoratibu mchakato ya kuifanya Simba kuingia katika mfumo wa hisa ambapo mfanyabiashara huyo alitoa ofa ya Sh bilioni 20 na katika zabuni hiyo hakupata mpinzani.

Tayari Mo Dewji ametangaza mikakati yake ya jinsi alivyopania kuifanya klabu ya Simba kujiendesha kisasa, akipanga kujenga viwanja viwili vya kisasa; kimoja cha nyasi bandia na kingine cha nyasi asili.

Pia, mfanyabiashara huyo amepanga kutoa kitita cha Sh bilioni moja kila msimu kwa ajili ya usajili wa wachezaji na Sh milioni 500 za benchi la ufundi.

Kitendo cha Simba kumkabidhi Mo timu, kimeonekana kuwagusa mno watu wa Yanga ambao nao wameamua kujibu mapigo kwa kumsaka mwekezaji mwenye uwezo wa kupiku dau la mfanyabiashara huyo kipenzi cha Wanamsimbazi na kuangukia kwa Mnigeria Dangote.

Alipoulizwa na BINGWA juu ya mpango wao huo, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, alikiri kuufahamu lakini akiweka wazi hana taarifa zaidi kwani huenda unatekelezwa kupitia kamati zao kadha wa kadha.

“Tuna kamati nyingi tulizozipa kazi za kushughulikia mambo mbalimbali, sasa huenda na hilo lipo chini ya moja ya kamati hizo, lakini ukweli ni kwamba hata mimi nimelisikia hivyo,” alisema.

Alilitaka gazeti hili kuwasiliana na mmoja wa maofisa wa Kamati ya Masoko ya Yanga, Salum Mkemi, kama anaweza kuzungumzia juu ya dili hilo linaloweza kuifanya Yanga kuwa moja ya klabu kubwa zinazoendeshwa kisasa zaidi barani Afrika.

BINGWA lilipomtafuta kwa simu Mkemi, alisema hafahamu lolote juu ya mpango huo na kwamba kama angekuwa anafahamu, asingesita kuweka wazi.

“Mimi sifahamu lolote juu ya mpango huo, kwanza sipo Dar es Salaam, nipo huku Mtwara,” alisema Mkemi.

Hata hivyo, wakati Mkemi akikana hilo, kitendo cha yeye kusema yupo mkoani Mtwara kunatia shaka huenda anafuatilia dili hilo kwani huko nako kuna ofisi za Dangote Cement kama alivyokiri mmoja wa maofisa wa kampuni hiyo aliyezungumza na gazeti hili jana.

Ofisa huyo wa Dangote Cement (jina tunalihifadhi), alisema kuwa binafsi hana taarifa kama Yanga wamewasilisha maombi yao kwa mwajiri wake, lakini akisisitiza kuwa iwapo wamefanya hivyo wanaweza kufanikiwa.

“Binafsi sina habari hizo maana tuna ofisi mbili (hapa Tanzania), moja ikiwa Dar es Salaam na nyingine Mtwara na makao makuu yapo Nigeria, sasa sijui hao Yanga wamepeleka maombi yao wapi. Ila uzuri ni kwamba Dangote mwenyewe anapenda sana mpira, hivyo iwapo Yanga watamuomba anaweza kuwasikiliza,” alisema.

Mtoa habari huyo hata hivyo alihoji, “Yanga wamewasilisha maombi ya mpango wao huo kwa Dangote Cement kama kampuni au Dangote mwenyewe kama mmiliki wa kampuni hiyo?”

Dangote amewahi kuhusishwa kutaka kuinunua Arsenal inayoshiriki Ligi Kuu England na timu ambayo ni mabingwa watetezi wa Kombe la FA.

Vuguvugu la mabadiliko ya uendeshaji wa klabu za Simba na Yanga limeonekana kupamba moto ikiwa ni baada ya Serikali kutoa mwongozo unaoelekeza kuwa wanachama wanatakiwa kuimiliki klabu kwa asilimia 51 na wawekezaji wengine asilimia 49
Bofya hapa kucheki video ya rosa Ree

Comments

Popular posts from this blog

Kubemenda Mtoto

Siwezi pitisha siku bila kutembea na malaya