Serikali yasogeza mbele tarehe ya kufunguliwa Shule za Azania, Jangwani na Milambo
- Get link
- X
- Other Apps
Serikali imelazimika kusogeza mbele tarehe ya kufungua shule kwa shule za Azania, Jangwani na Milambo kutokana na Wakala wa Majengo(TBA), kushindwa kumaliza ukarabati huo kwa muda uliotakiwa.
Uamuzi huo ulifikiwa jana Jumamosi jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Leonard Akwilapo alipokutana na walimu wa shule hizo na viongozi wa Manispaa ya Ilala.
Akwilapo alisema kitendo hicho hakijamfurahisha na kuahidi kufuatilia kwa mara nyingine mkataba wa namna ya utekelezaji wa ukarabati huo walioingia Wizara na TBA.
"TBA mnapaswa kujua mmepewa jukumu hili kwa kuwa Serikali imewaamini, lakini hii isiwe kisingizio cha nyie kuvurunda kwa kisingizio tu ni taasisi ya Serikali nitapitia tena upya na mwanasheria wetu mkataba tulioingia kuona ni wapi watu hawakutekeleza wajibu wao na hatutasita kuchukua hatua tutakapobaini kuna tatizo," alisema.
Hata hivyo, alisema pamoja na kuongeza siku hizo ambapo sasa badala ya kufungua shule kesho Jumatatu, watafungua Januari 22, hataongeza siku zaidi na kuwahakikishia walimu kwamba muda walioupoteza wa ratiba za kufundisha zitafidiwa katika likizo ya Aprili na ile ya Juni.
Akijibu sababu zilizowachelewesha kumaliza ukarabati huo kwa muda, Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Dar es Salaam, Manasseh Shekalaghe alisema zipo sababu nyingi zilizochelewesha ikiwemo gharama kuongezeka tofauti na ilivyodhaniwa awali.
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment