JOHARI AFUNGUKA SIRI YA KIFO CHA MAMA YAKE
MREMBO wa filamu za Kibongo, Blandina Chagula ‘Johari’ ameanika siri ya kifo cha mama yake kwa kueleza namna ambavyo alipigana kutetea kifo cha mama yake mzazi.
Johari alipata pigo hilo usiku wa kuamkia Jumatano iliyopita katika Hospitali ya Hindu Mandali, jijini Dar es Salaam baada ya mama yake kulazwa kwa ugonjwa wa kisukari kwa saa chache tangu afikishwe hospitalini hapo.
Kabla ya kupatwa na umauti huo, Johari alikuwa akiishi na mama yake mzazi, maeneo ya Gereji, Mabibo jijini Dar ambapo kwa zaidi ya miaka mitatu, msanii huyo alihangaika kutetea uhai wa mama yake, kwa nyakati tofauti.
Katika kipindi chote hicho, Johari alikuwa mzito sana kuelezea mateso aliyokuwa anayapitia mama yake, zaidi alikuwa akiwaelezea watu wake wa karibu sana. Akizungumza na Risasi Jumamosi, akiwa kwenye nyumba ya familia, Mburahati jijini Dar, Johari alisema kifo cha mama yake kimekuwa pigo kubwa kwake na kueleza namna alivyopambana kumpigania.
“Nimehangaika jamani. Nilikuwa silali, mchana na usiku nilikuwa nikipambana kuhakikisha naokoa maisha ya mama yangu. “Unajua alikuwa kuna wakati anakuwa na hali nzuri, kuna wakati ndio hivyo kikipanda, hali inakuwa mbaya sana. Kwa miaka zaidi ya mitatu nimekuwa nikipambana na afya ya mama yangu,” alisema Johari huku akilengwalengwa machozi.
Akizungumza kuhusu ratiba ya mazishi Jumatano iliyopita, muigizaji Salum Mchoma ‘Chiki’, ambaye alichaguliwa kuwa msemaji wa familia, alisema siku ya Alhamisi (juzi), mwili wa mama yake Johari ungefikishwa nyumbani hapo kisha ungepelekwa Msikitini wa Mbukusi, Mburahati baadaye kuzikwa katika Makaburi ya Kisutu jijini Dar. Msiba huo ulihudhuriwa na waigizaji wengi akiwemo, Vincent Kigosi ‘Ray’, Ndambangwe Misayo ‘Thea’, Sabrina Rupia ‘Cathy’, Nuru Nassor ‘Nora’ na wengine wengi
Comments
Post a Comment