WASIOKUWA NA VITAMBULISHO VYA UTAIFA HAWATARUHUSIWA KUTUMIA SIMU.


MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imebainisha kuwa haitakuwa rahisi kwa mtu yoyote raia wa Tanzania kumiliki simu kama hatakuwa na kitambulisho cha Taifa.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano NIDA, Rose Mdami, alisema pamoja na mambo mengine kwa sasa mamlaka hiyo inaendelea na usajili wa wananchi katika mikoa 20 ya Tanzania Bara, huku kwa upande wa Zanzibar zoezi likiwa limekamilika.
Akizungumzia maendeleo ya uandikishaji huo, Rose alisema kuwa NIDA inaendelea kusajili Mamlaka za Udhibiti wa mifuko ya Hifadhi za Jamii (SSRA) kwa lengo la kusajili wanachama na wanufaika wote wa mifuko hiyo nchini.
Mbali ya zoezi hilo, Rose alisema pia wanaendelea kulifanyia kazi ni usajili wa kampuni za simu kwa sababu wateja wote wapya wa kampuni zote watakaotaka kusajili laini mpya watalazimika kuwa na vitambulisho vya taifa.
“Majaribio ya zoezi hilo yanafanyika katika mikoa sita, kwa Dar es Salaam ni Mliman City, hivyo wananchi wanaokwenda kusajili laini za simu kama hawana vitambulisho vya taifa basi wanashauriwa kwenda kwenye ofisi za NIDA wilaya ili wapate vitambulisho kwa sababu mfumo utakuwa unamtambua mtu kwa alama za vidole.”
Mbali ya kumiliki simu, lakini pia haitakuwa rahisi kupata leseni za biashara na kusajili majina ya kampuni chini ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) bila ya kuwa na kitambulisho cha Taifa.
“Jambo jingine ni kwamba huwezi kupata hati ya kusafiria (Passport) kama huna kitambulisho cha Taifa, kwahiyo kazi tunayoifanya kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji ni kuhakikisha wananchi wote wanaotaka kupata Passport wanakwenda kwenye vituo vyetu vya usajili na kuna utaratibu maalum wa kuwasaidia wenye safari za dharura ambao unamwezesha kupata kitambulisho kwa wakati.”
GHARAMA ZA MRADI
Akizungumzia gharama za mradi huo Rose alisema mradi hadi kukamilika unategemea kugharimu kiasi cha dola za Marekani 149 milioni, ambazo ni wastani wa sh. 335.3 bilioni.
Rose alisema katika awamu hii ambayo inaendelea NIDA inawafuta wananchi katika ngazi ya Kata, vijiji na mitaa, lakini baada ya awamu hiyo kwisha watakaohitaji watatakiwa kwenda katika ofisi za mamlaka hiyo ngazi ya wilaya.
“Hali ya usajili kwa nchi nzima ni nzuri kwani tunaendelea na zoezi hilo kwenye mikoa 20 ya Tanzania Bara na kuanzia Machi 19 mwaka huu tumeanza usajili katika mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma, uzinduzi rasmi utafanyika hivi karibuni.
“Katika awamu hii tunawafikia wananchi katika ngazi ya Kata, Vijiji na Mitaa, lakini kwa wale ambao hawatasajiliwa watalazimika kwenda katika ofisi za NIDA ngazi ya wilaya,” alisema Rose.
Alisema pamoja na usajili wa wananchi NIDA inaendelea na zoezi la kuwasajili wafanyabiashara na wachimbaji katika mgodi wa Mererani mkoani Arusha.
“Ukuta katika Mgodi wa Tanzanite unakaribia kumalizika na kwa makubaliano tuliyoyafanya na Wizara ya Madini ni kwamba watu wote watakaokuwa wanafanya shuguli zao ndani ya mgodi huo watapaswa kutumia vitambulisho vya taifa, kwahiyo usajili kwa wachimbaji wote wakubwa kwa wadogo uko mbioni kumalizika.
“Ninaposema wachimbaji wakubwa na wadogo nina maana ya kwamba NIDA inatoa vitambulisho vya aina tatu ambapo kuna kitambulisho cha Raia, Mgeni na Mkimbizi. Hivyo wageni wanaofanya shuguli zao watasajiliwa kulingana na taratibu ambazo zimewekwa, ili wote wanaoingia kwenye machimbo hayo watumie vitambulisho vya taifa,” alisema.
AGIZO LA RC MARA
Kuhusu agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima la kuwataka wakazi wote wa mkoa huo kuhakikisha wanasajiliwa ndani ya miezi mitatu ya zoezi, Rose alisema kuwa agizo hilo limesaidia kutekelezwa kwa zoezi hilo kwa asilimia 94.
Alisema kuwa Mkoa wa Mara ni kati ya mikoa ambayo NIDA ilianza zoezi hilo Novemba 22, mwaka jana kwa kipindi cha miezi mitatu.
“Februari 22 mwaka huu tulifunga rasmi zezi hilo katika mkoa huo kwa maana ya kwamba tulisajili asilimia 94 sawa na wananchi 718,647 kati ya 763,142 ya watu ambao walitakiwa kusajiliwa.
“Kinachoendelea sasa hivi ni kuchakata zile taarifa ambapo baada ya hapo uzalishaji utafanyia na makubaliano ni kwamba ifikapo katikati ya Aprili tutaanza kugawa vitambulisho kwa wale ambao watakuwa wamekidhi vigezo.
“Kwahiyo maelekezo yaliyotolewa yamesaidia, kwa sasa wananchi wanaendelea na mapingamizi ambapo kamati za ulinzi na usalama zinakaa na kupitia maombi ya wote walioomba vitambulisho ili kijiridhisha kama wote ni raia wa Tanzania,” alisema Rose.

Comments

Popular posts from this blog

Kubemenda Mtoto

Siwezi pitisha siku bila kutembea na malaya

HAYA NDIO MADHARA YA KUFANYA MAPENZI KWA NJIA YA MDOMO. (Oral sex).