PANYA ROAD WAILUKU WAVAMIA NA KUPORA MALI.
Kwa mara nyingine tena taharuki, hofu na wasiwasi mkubwa viliwakumba wakazi wa Tabata wilayani Ilala jijini Dar es Salaam kwa takribani saa tatu baada ya kundi maarufu la uporaji la Panya Road kuvamia mitaa mbalimbali na kupora mali. Kundi hilo lililokuwa na vijana zaidi ya 30 waliokuwa wameshika nondo, visu, mapanga na bisibisi jana usiku Machi 29,2018 lilisababisha wakazi wa Tabata Kisiwani, Kimanga hadi Kinyerezi kujifungia majumbani mwao na baadhi kujifungia ndani kutokana na jinsi kundi hilo lilivyokuwa likivamia biashara na nyumba kupora. Mmoja wa mashuhuda wa eneo la Tabata Kisiwani, Isaya Subi amesema tukio hilo lilianza saa mbili usiku ambapo kundi hilo lilivamia katika eneo hilo, kupora mali mbalimbali kwenye maduka pamoja na kuwapora wapita njia. “Vijana hawa si mchezo walikuwa kama 30 hivi kila mmoja alibeba nondo, bisibisi, wembe na spoku wakikukuta njiani wanakupiga huku wakikusachi na kuchukua kila kitu ulichokuwa nacho wengine walivamia maduka na kuchukua bidhaa...