Dili la HIMID MAO na NGASA Kutumia yanga

CLARA ALPHONCE NA SAADA SALIM

BAADA ya Kamati ya Usajili ya Klabu ya Yanga kumalizana na kiungo wa Mbeya City, Rafael Daud, uongozi wa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara umepanga kufanya jambo kubwa katika usajili wiki hii.
Mmoja wa wachezaji ambao wanatajwa kuwa watasajiliwa na klabu hiyo wiki hii ni Himid Mao wa Azam FC, kwani Yanga wana mpango wa kufanya mazungumzo na uongozi wa Azam ili waweze kufikia mwafaka na kumsajili.

Taarifa ambazo tumezi pata zinadai kuwa, Kocha Mzambia, George Lwandamina, juzi alikutana na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hussein Nyika, na kuzungumza naye masuala ya usajili, ikiwamo  kusisitiza usajili wa Mao.

Chanzo hicho kimedai kuwa, Yanga wakimalizana na Azam, Mao ataonekana uwanjani rasmi Agosti 5, mwaka huu, timu hiyo itakapomenyana na Singida United katika mchezo wa kirafiki, ambao winga wake wa zamani, Mrisho Ngassa, pia anatajwa atakuwapo.

Tulipomtafuta Nyika kuzungumzia mchakato wa usajili unaoendelea, alisema wanatarajia kuongeza wachezaji wawili, ambao ndio watafunga zoezi hilo msimu huu.

Alisema mchezaji mmoja atasajiliwa katikati ya wiki na mwingine ni mwishoni mwa wiki, ambapo washamsainisha uwanjani baada ya mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Singida United.

“Siwezi kuweka wazi kuwa ni wachezaji gani tunaowasajili, hiyo ni ‘surprise’, hivyo subiria siku hiyo utajua akina nani,” alisema Nyika.

Kuhusiana na usajili wa Mao, Nyika alisema mchezaji huyo si mbaya, kwani wakimpata atawasaidia kwenye timu yao.

“Mfano wewe ungekuwa kocha ungemkataa kweli mchezaji kama Himid? Hivyo kama kocha atatuambia anamuhitaji tutamsainisha,” alisema Nyika.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Azam, Idrissa Nassor ‘Father’, alisema mpaka sasa hakuna timu iliyokwenda kwao ikihitaji kufanya mazungumzo yanayomhusu kiungo wao, Mao.

Alisema Mao bado ni mchezaji wao halali na juzi alijiunga na wenzake kwa ajili ya mazoezi yanayoendelea katika Uwanja wa Azam Complex, kujiandaa na Ligi Kuu msimu ujao.

“Si Yanga wala timu yoyote kutoka nje iliyokuja kwetu kutaka kufanya mazungumzo ya kumsajili Mao,” alisema Father

Comments

Popular posts from this blog

Kubemenda Mtoto

Siwezi pitisha siku bila kutembea na malaya