Baada ya kufungwa Jana Yanga yashika nafasi ya mwisho.
Mabingwa wa soka nchini Yanga, wamepoteza mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ugenini dhidi ya U.S.M Alger kwa mabao 4-0 na kushika mkia katika kundi la la D.
Mchezo huo uliopigwa usiku wa kuamkia leo jijini Algiers, Yanga iliruhusu mabao mawili katika kipindi cha kwanza kabla ya kuongezwa mengine mawili kipindi cha pili na kufanya waondoke bila alama huku wakiwa na deni kubwa la mabao ya kufungwa.
Katika Kundi D, Yanga inashika nafasi ya nne ambayo ni ya mwisho baada ya mechi nyingine ya kundi hilo iliyopigwa usiku huo huo kati ya wenyeji Rayon Sport ambao walitoka sare ya bao 1-1 na Gor Mahia ya Kenya kwenye Uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali.
Kwenye ligi kuu Tanzania Bara, Yanga inashika nafasi ya tatu nyuma ya Simba na Azam FC ikiwa na alama 48 kwenye mechi 24 ilizocheza hadi sasa. Azam ina alama 49 kwenye mechi 27 na Simba ina pointi 65 baada ya mechi 27.
Kundi D sasa linaongozwa na U.S.M Alger yenye alama 3 ikifuatiwa na Gor Mahia yenye alama 1 sawa na Rayon Sports yenye alama moja pia huku Yanga ikiwa haina alama baada ya kupoteza mechi yake.
Comments
Post a Comment