LICHA ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga kuiondosha Timu ya Ihefu FC kwenye mashindano ya kombe la shirikisho, Kocha msaidizi wa Wanajangwani hao, Shadrack Nsajigwa, amewanyooshea mikono Ihefu kutokana na kiwango walichoonyesha. Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, Nsajigwa alikiri vijana hao kutoka katika mabonde ya Mpunga wilayani Mbarali kuonyesha mchezo mzuri kuliko Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa. Alisema timu hiyo iliyojaa vijana, ilicheza vizuri na kwa nguvu katika dakika zote 90 na kwamba Yanga wao walianza kuonyesha mchezo mzuri katika dakika 45 za kipindi cha pili. “Nafurahi tumepata ushindi unaotufanya tusonge mbele katika mashindano haya, lakini vijana wa Ihefu wameonyesha mchezo mzuri kuliko sisi na wamecheza kwa nguvu muda wote, penalti ni bahati na yeyote anaweza kukosa,” alisema Nsajigwa. Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Ihefu FC, Michael Kasegey...